UWINGI-TAALUMA WA BEMBELEZI ZA WASWAHILI
Abstract
Dhana ya uwingi-taaluma ina maana ya kuunganisha au kuhusisha ujuzi
anuwai wa kitaaluma katika mtazamo wa mada au tatizo. Mkabala wa
uwingi-taaluma hulenga kueleza tatizo nje ya mipaka ya kawaida kwa
kuungwa mkono na mikabala tofauti kutoka taaluma mbalimbali na kufikia
suluhu zilizo na misingi yake katika uelewa wa hali changamano (Koski na
Savolainen, 2016). Bembelezi za Waswahili zinaakisi uchangamano huo;
kwamba zinaonekana kuwa na majukumu anuwai katika jamii. Majukumu
kama vile ya utakasaji hisia, mawasiliano, uelimishaji halikadhalika uadilishaji.
Majukumu haya ndio yanayoibua hisia kwamba zina uwingi-taaluma na hivyo
kuwavutia watafiti kuchunguza taaluma mbalimbali zilizomo. Utafiti
uliongozwa na nadharia ya uwingi-taaluma kwa mujibu wa Al-Saleem (2018).
Data za bembelezi za Waswahili zilikusanywa katika Kisiwa Faza. Washiriki 11
wa kike wenye umri kati ya miaka 18 na 65 waliteuliwa kwa kuelekezwa na
mmoja akateuliwa kimaksudi ili kusailiwa. Vikundi lengwa viwili vya mjadala,
kila kimoja kikiwa na wasailiwa sita viliundwa kwa misingi ya umri, na data ya
bembelezi 20 ikakusanywa kutokana na vikundi hivyo. Hatimaye bembelezi
10 ziliteuliwa kimaksudi ili kuchunguza uwingi taaluma uliomo. Data
zilichanganuliwa kimaelezo. Matokeo ya utafiti yalionyesha dhahiri kwamba
bembelezi zina uwingi-taaluma na hutumiwa katika miktadha ya shule,
nyumbani, matibabu na mingineyo. Utafiti huu unatoa mchango wa kiusomi
kwa watafiti wajao wa fasihi simulizi, wataalamu wa masuala ya elimu,
wahudumu wa afya, wanasaikolojia na wanataaluma wengineo hususan wa
taaluma zilizoshughulikiwa katika makala haya.
URI
https://doi.org/10.51317/eajk.v4i1.737http://repository.mut.ac.ke:8080/xmlui/handle/123456789/6555